Mambo ya uwajibikaji hayana mwisho. Watanzania pale Uingereza, abiria wa basi huko Mikumi wote wanaomba uwajibikaji. Sasa wafadhili kutoka nje, wanataka kuwasaidia vyombo vya habari kuomba uwajibikaji. Mambo kibao yatakuwepo – mafunzo, skolashipu, exchange visits na misaada.

Serikali za Uswisi, Ireland, UK, Denmark, Netherlands na Canada wameamua kuandaa Tanzania Media Fund (haina jina la kiswahili). Mfumo huu unategemea kuanza rasmi baada ya miezi kadhaa. Utakuwa na lengo hili:

The overall objective of the programme is to increase the quantity of quality public (PJ) and investigative (IJ) products that better inform the public, contribute to debate and thereby increase public demand for greater accountability across Tanzania

Terms of Reference kwa shirika italoendesha mfumo huu ziko hapa, bonyeza tu. Maelezo zaidi yanapatikana huku na huko.

Kwa ufupi, Tanzania Media Fund itatoa msaada kwa namna tatu: mafunzo kwa waandishi wa habari; kufadhili uandishi wa uchunguzi, au ‘investigative journalism’ na kuandaa Legal Defence Fund

Kwa upande wa mafunzo, sina tatizo – ni muhimu, yanahitajika.

Lakini kwa kufadhili uandishi wa uchunguzi, nina wasiwasi. Swali la kwanza: je, miaka ya hivi karibuni, kiasi cha uandishi wa aina hii umepungua au umeongezeka?

Kwa uzoefu wangu, kwa takriban miaka kumi, uandishi wa uchunguzi umeongezeka bila shaka (kama gini co-efficient, lakini hili ni suala lingine).

Nitoe mifano michache ya mwaka huu:

  • Ujenzi wa Benki Kuu Ya Tanzania (Mwananchi)
  • Commercial Debt Scandal ya Benki Kuu ya Tanzania (kwanza kwenye Mwananchi, na jana kwenye Daily News)
  • Quality Plaza (This Day)
  • Biashara ya Rais Mkapa alipokuwa Ikulu (This Day/Kulikoni)

Miaka kumi iliyopita, usingesoma habari za aina ile. Inaonyesha kwamba vyombo vya habari vya Tanzania vinakua, vinaendelea na uandishi wa aina hii, bila kusaidiwa na wafadhili kutoka nje.

Terms of Reference zinaeleza kuwa wafadhili wanategemea kuona:

At least x no. of individuals and x no. of agencies funded annually to carry out pieces of journalism resulting in a minimum of x no. of investigative and pubic journalism pieces published and broadcast.

Tufikirie mradi huu zaidi…. Mwandishi wa habari mmoja akitaka kuchunguza skendo fulani, itabidi aandike proposal ya kuomba fedha. Ataituma kwa Tanzania Media Fund. Maafisa wao wataisoma, wataipeleka kwa ‘Steering Committee’. Watakubali au hawatakubali. Je, ukitaka kuchunguza suala la kigogo fulani na shughuli zake, utasambaza hapa na pale kwa namna hii?

Je, akisikia kuwa kuna skendo inayohusu wafadhili, atachunguza? Au, atakataa kwa sababu anawategemea kwa mafunzo na msaada?

Swali la mwisho: je, vyombo vya habari vya Tanzania vitegemee wafidhili kutoka Ulaya?

Ukitaka kufikiria zaidi mambo ya uandishi wa uchunguzi, soma hii, inayohusu ukosefu wa uandishi wa aina hii China. Ukisoma uandishi wa mwaka jana wa Ndesanjo Macha, utatafakari zaidi.