Je, mwanablogu akiweka nakala kwenye blogu yake, nakala ni mali ya nani?

Namna moja ya kuboresha mtandao wa wanablogu ni huduma ya ‘aggregators’. Mimi mwenyewe nimeungana na Afrigator. Nikiweka nakala, kichwa chake kitawekwa kwenye tovuti ya Afrigator. Kichwa chake kikivutia, ukibonyeza tu, utapelekwa hapa hapa kwa kifimbocheza. Karibu sana.

Jumuwata wanaandaa aggregator kwa wanablogu wa Tanzania, lakini bado tunasubiri matokeo ya kazi zao.

Kwa sasa, Jambo Blog Network imeanza. Ukiwatembelea akina-JBN, utaona vichwa vya nakala nyingi ambazo zimeandaliwa na wanablogu mbalimbali hapa Tanzania. Kwa mfano, leo kwenya JBN nimeona ‘Demokrasia Ya Kijambazi Kenya‘. Ukibonyeza utapelekwa kwenye ukarasa mwingine wa JBN. Utaona matangazo manane (ya magari kutoka Japan, viwanja, hata Mungu).

Ukibonyeza Demokrasia Ya Kijambazi Kenya hapa, utapelekwa kwenye nakala halisi ya Ndesanjo Macha. Hamna matangazo – utasoma mawazo ya Ndesanjo tu.  Kama wanablogu wengi, ameyatangaza bure kwenye blogu yake. Lakini kwenye JBN, nakala yake ni chanzo cha kupata kipato.

Nisiwe mkali sana kwa akina JBN. Lakini naomba wafikirie zaidi namna wanavyounganisha blogu za Tanzania.

Nikisoma nakala hii kwenye JBN, nitaona matangazo mangapi? Pia, je, mimi nitapata asilimia kumi ya kipato cha matangazo?