Kwa maoni yangu, kuna mashirika machache yasiyo ya serikali ambayo yanajitahidi kuleta mawazo mapya na vitendo vipya hapa Tanzania. Na HakiElimu ni mojawapo. Wamesema mambo mengi ya ukweli mpaka walipigwa marufuku….. Heshima kwao. Wapo kwenye mstari wa mbele katika kulinda haki za wananchi na kutuhamasisha.

Lakini, hivi karibuni, karibu kila mara mimi huwasha luninga yangu, huona nembo yao. “The Week in Perspective” kwenye TVT, “City Sounds” kwenye EATV, “Kipima Joto” cha ITV, kipindi kile kipya cha kutoka Dodoma kwenye TVT, juma mosi mchana….. nembo yao inaonekana karibu kila siku.

Nilitembelea tovuti yao kupata maelezo zaidi, nikapata taarifa yao ya 2005, ambaye inapatikana hapa. Nilishangaa kujua kiasi HakiElimu inashawishi vyombo vya habari. Kwa mwaka 2005, walifadhili zaidi ya taarifa 200 kwenye magazeti, luninga na redio. Pamoja na hizo, walifadhili “Sema Usikike” (ITV), “Mgongano wa Mawazo” (ITV), “Elimu Maalum” (RTD) na “Sauti ya Watu” (TVT).

Upande wa kazi yao kwa vyombo vya habari, lengo la HakiElimu ni

The voices of ordinary people regarding education and democracy are investigated and independently reported, and this has led to greater awareness, accountability and public action.

Mimi nakubaliana na lengo hili kw asilimia mia moja. Pia, nimefurahi kuwa HakiElimu wanajitahidi kutusogeza mbele. Wasiwasi wangu ni kwamba, athari yao kwa vyombo vya habari ni kubwa sana mpaka itawezekana kupunguza uhuru wa vyombo vya habari na siyo kujenga uhuru wake. Demokrasia na uhuru wa ukweli unategemea sauti mbalimbali na maoni tofauti. Naogopa kuwa sekta ya uandishi wa habari hapa Tanzania unategemea sana wafadhili kutoka nje, kama serikali na ile sekta ya “NGOs”.

Tusisahau kuwa karibu fedha zote za HakiElimu zinatoka mashirika ya kimataifa yasiyo ya serikali na serikali za nchi za nje. Ili kupata hela, kwanza inabidi wawashawishi wafadhili hawa na kukubaliana na malengo ya wafadhili. Na waandishi wa habari, je? Ili kupata hela, kwanaza inabidi wawashawishi mashirika kama HakiElimu kuwa wanakubaliana na malengo yao. Na katika uhusiano wa kimataifa (hata katika maisha kwa ujumla) matajiri wana ushawishi mkubwa zaidi kuliko wanyonge.

Je wakati wa ukoloni tulikuwa na vyombo huru vya habari? Je, wakati wa Nyerere, tulikuwa na vyombo huru vya habari? Siku hizi, je, tunasikia sauti za nani?

Advertisements