Mada ya leo ni Benjamin, siyo Richard. Wiki ijayo, tutajua nani atazawadiwa dola milioni tano kwa kuwa kiongozi bora – dola laki tano kila mwaka kwa miaka kumi, na dola laki mbili kila mwaka baada ya hapo mpaka kifo (dola za Amerika, siyo Hong Kong). Washindani ni wengi, kumi na tatu, mmojawapo ni Rais Mstaafu Mheshimiwa Benjamin William Mkapa. Sitaki kutafakari matatizo yake leo, bora tuzungumze kuhusu zawadi hiyo kwa ujumla.

Mchezo huu umefadhiliwa na Mo Ibrahim. Lengo la mchezo huu ni kuwatia moyo viongozi ambao wameendeleza utawala bora katika nchi zao. Sioni tatizo kwa suala la utawala bora. Nadhani sote tungefurahia utawala wa aina hii. Lakini kwanini hapa Afrika, inaonekana kuwa viongozi wanahitaji kulipwa ili kutoiba mali ya nchi, kukubali matokeo ya uchaguzi, na kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari? Je, Meles Zenawi ataacha unyama wake pale Ogaden akiona fursa ya kupewa zawadi hiyo?

Mwanzoni, nilisema kuwa sitaki kutafakari matatizo ya Rais Mstaafu Mkapa. Lakini, si mbaya kulinganisha kidogo. Thamani ya zawadi ni USD5 milioni. Thamani ya kamisheni ya dili ya rada, ilikuwa USD12 milioni.

Advertisements