networks


Rais Kikwete alitoa hotuba mbili mwezi uliopita. Kwanza, aliongea na Wazee wa Dar es Salaam, Diamond Jubilee Hall. Mwisho wa mwezi, tulisikia hotuba yake ya kufunga mwezi.

Alivyosema Rais kwenye hotuba yake kwa wananchi kwa mwezi wa pili, ulikuwa “mwezi wa matukio makubwa ya kukumbukwa kwa miaka mingi ijayo”. Bado haipatikani kwenye tovuti ya serikali, lakini ipo kwa Michuzi. Bonyeza hapa. Kwa hotuba kwa Wazee, bonyeza hapa.

Kuhusu Richmond, Mh. Rais hajakosea – tuliona matukio makubwa. Lakini baada ya kusikiliza na kusoma hotuba zake, nadhani angefurahi tuyasahau. Soma yafuatayo:

Nchi yetu ilipata mtikisiko mkubwa na wananchi wengi walikuwa katika hali ya mkanganyiko, wakati mwingine walikuwa wakijiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu kuhusu hatma ya taifa letu.

Siyo siri, tumejiuliza maswali mengi. Lakini kutoka kwa Rais mwenyewe, hamna majibu. Alitusimulia kuhusu vikao vya Kamati ya Uongozi ya Chama na Kamati ya Wabunge wote wa CCM baada ya ripoti ya Mwakyembe kuwasilishwa. Najiuliza, je, walijadiliana nini? Taarifa za vikao zilipendekeza nini? Au, kusema wazi, nani alimlinda nani katika majadiliano hayo?

Wengi wamejiuliza maswali, hasa kuhusu Lowassa, harakati zake na mahusiano yake na Rais. Rais mwenyewe amlisemaje?

Napenda kuitumia nafasi hii kumshukuru sana Mhe. Edward Lowassa kwa moyo wake wa uzalendo na kwa utumishi wake kwa taifa letu. Ameitumikia nchi kwa jitihada kubwa katika nyadhifa mbalimbali mpaka kufikia kuwa Waziri Mkuu. Katika miaka hii miwili amefanya kazi kubwa ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo la taifa letu. Ameacha alama za kudumu za kipindi chake cha miaka miwili. Yaliyotokea ni ajali katika maisha ya siasa, lakini naamini historia itamhukumu kwa haki stahiki

Zaidi ya hapo, ametuambia kuwa:

Nchi yetu tayari imerudia hali yake ya kawaida na kila mmoja wetu anaendelea na shughuli zake.

Yaani, sina maneno ya kuelezea mshtuko wangu kwa maneno hayo. Waziri Mkuu, ameomtuhumiwa kwa ufisadi mkubwa kupita kiasi, na pia amekosa heshima kwa wananchi atahukumuliwa na historia! Aidha, sisi tunaendelea na shuguli zetu bila wasiwasi baada ya kutulizwa na Rais. Je, Rais alikuwa anamlenga nani kwa maneno hayo? Wananchi? Wazee? Au wenzake wa Chama?

Kwenye hotuba yake ya kufunga mwezi, hana usemi kuhusu mambo hayo. Rais ameendelea na shughuli zake za kumpokea Bush na kutembelea Kenya. Basi. Wakati huo huo, Waziri Mkuu aliyejiuzulu, amejifagilia kwenye TVT.

Mwisho wa mwezi, tulichanganyikiwa na mambo ya Jambo Forums. Utakumbuka kuwa tovuti hiyo ilifungwa kwa muda, na watu wawili walikamatwa. Kitu kinachosikitisha ni hiki: kwanini imebidi tutegemee shirika kutoka nje (Committee to Protect Journalists) kupata taarifa nzima na wazi ya kashfa hiyo. Soma makala yao hapa. Tumepata kila kitu – majina, sababu za kukamatwa, hadi jina la mwanasheria wao (Tundu Lissu, mwanasheria wa CHADEMA).

Matukio ya Richmond na Jambo Forums yametuonyesha kuwa safari ya kufikia uwazi na ukweli hapa Tanzania bado ni ndefu.

Advertisements

Je, mwanablogu akiweka nakala kwenye blogu yake, nakala ni mali ya nani?

Namna moja ya kuboresha mtandao wa wanablogu ni huduma ya ‘aggregators’. Mimi mwenyewe nimeungana na Afrigator. Nikiweka nakala, kichwa chake kitawekwa kwenye tovuti ya Afrigator. Kichwa chake kikivutia, ukibonyeza tu, utapelekwa hapa hapa kwa kifimbocheza. Karibu sana.

Jumuwata wanaandaa aggregator kwa wanablogu wa Tanzania, lakini bado tunasubiri matokeo ya kazi zao.

Kwa sasa, Jambo Blog Network imeanza. Ukiwatembelea akina-JBN, utaona vichwa vya nakala nyingi ambazo zimeandaliwa na wanablogu mbalimbali hapa Tanzania. Kwa mfano, leo kwenya JBN nimeona ‘Demokrasia Ya Kijambazi Kenya‘. Ukibonyeza utapelekwa kwenye ukarasa mwingine wa JBN. Utaona matangazo manane (ya magari kutoka Japan, viwanja, hata Mungu).

Ukibonyeza Demokrasia Ya Kijambazi Kenya hapa, utapelekwa kwenye nakala halisi ya Ndesanjo Macha. Hamna matangazo – utasoma mawazo ya Ndesanjo tu.  Kama wanablogu wengi, ameyatangaza bure kwenye blogu yake. Lakini kwenye JBN, nakala yake ni chanzo cha kupata kipato.

Nisiwe mkali sana kwa akina JBN. Lakini naomba wafikirie zaidi namna wanavyounganisha blogu za Tanzania.

Nikisoma nakala hii kwenye JBN, nitaona matangazo mangapi? Pia, je, mimi nitapata asilimia kumi ya kipato cha matangazo?

Ukipata nafasi, tembelea blogu ya Jumuwata. Wameomba tuchangie mawazo yetu kuhusu katiba mpya ya Jumuwata.

Hapa Tanzania, tumezoea kushirikiana kwa mabaya na mazuri. Lakini Jumuwata ni kitu kipya, ambacho tunajitahidi kushirikiana bila kukutana rasmi.  Sote tumekaribishwa. 

Hivi karibuni, nilibahatika kutembelea tovuti ya Mheshimiwa Nimrod Mkono. Inaonekana hapa. Mh. Mkono ni mbunge wa Musoma Vijijini. Napendekeza utembelee tovuti hiyo. Inaonyesha vizuri kazi ya mbunge hapa Tanzania.

Sina mabaya ya kusema. Inaonekana kuwa Mh. Mkono anajitahidi kuendeleza jimbo lake, hasa upande wa elimu. Lakini si mbaya kuuliza maswali machache….

Kwanza, kwanini tovuti hii imeandikwa kwa kiingereza? Je, lengo lake ni kuwasiliana na wananchi au kuwasiliana na wafadhili kutoka nje?

Pili, baada ya kustaafu Mh. Mkono, nani ataendesha miradi hiyo pale Musoma?

Tatu, je, kwanini haijaandikwa kuwa Mh. Mkono ni mbunge upande wa CCM? Asifiche kitu hicho. Kuchaguliwa na wananchi ni heshima.

Si kila jimbo lina mbunge mwenye uwezo kama Mh. Mkono. Je, wananchi wategemee uwezo wa mbunge wao kuliko serikali wakitaka maisha bora?

Kwa kumalizia, niseme kwamba nimefurahi kuwa mbunge mmoja anatumia teknolojia ya mtandao pamoja na mtandao wake binafsi.

Namshukuru Jaduong Metty kwa kunihamasisha kuhusu Mh. Mkono na kazi zake mbalimbali.